CHADEMA WAMTAKA RAIS DK. MAGUFULI KUELEZA SABABU ZA KUTENGUA NAFASI YA UWAZIRI WA NAPE NNAUYE
Makamu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu chama hicho kuwateuwa Lawrence Masha na Ezekia Wenje kugombea Ubunge wa Afrika Mashariki pamoja na mambo mbalimbali yayoendelea nchini. Kulia ni Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.
Na Dotto Mwaibale
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemtaka Rais Dk. John Magufuli kuueleza umma wa Watanzania sababu za kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.
Katika hatua nyingine kimesema wabunge wa vyama pinzani kwa kushirikiana na wabunge wa Chama cha Mapinduzi wanatarajia kuwasha moto katika Bunge la Bajeti linalo tarajia kuanza mapema mwezi ujao kulingana na mambo mbalimbali yautendaji wa Serikali ya awamu ya tano.
Aidha chama hicho kimemtaka Rais Magufuli kumchukulia hatua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutii matakwa ya wananchi na kuepuka hali ya kuonekana kutumia vibaya madaraka kwa kuwahukumu baadhi ya watu kwa kuwalinda watu wenye makosa ya wazi wazi.
Akizungumza Makao Makuu ya chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam leo siku moja baada ya kutenguliwa kwa uteuzi huo Naibu Katibu Mkuu wa chama cha Chadema Bara, John Mnyika alisema kutokana na taarifa ya Ikulu kutoeleza sababu za kutenguliwa kwa nafasi ya Nape hivyo ipo haja kwa Rais kueleeza wazi sababu ya kumuondoa.
"Rais anapaswa kujitokeza kutoa sababu kwanini katika kipindi hichi ambacho kamati iliyoundwa na Waziri kutoa taarifa iliyoeleza wazo makosa yaliyofanywa na Makonda katika siku chache baada ya Rais kumkingia kifua," alisema.
Alifafanua kuwa hatua ya Rais Mgufuli kumuondoa Nape ni matumizi mabaya na ya wazi ya madaraka katika kuwahukumu baadhi ya watu na kuwalinda watu ambao wanafanya makosa ya wazi wazi.
"Chimbuko la matatizo haya ni Mkuu wa Mkoa huo na kauli za Rais Magufuli katika kipindi cha siku za karibuni kuhusiana na Makonda kwa gharama yeyote ya kumlinda Makonda ni wazi kwamba ni matumizi mabaya madaraka," alisema.
Hata hivyo alisema kuwa matumizi hayo mabaya ya madaraka kwa sasa yamejipenyeza zaidi hali ambayo kwa sasa hayamuhusu Rais Pekeake bali hata watendaji wa vyombo vya dola ambavyo pia vimejidhihirisha kutokana na matukio yanayoendelea ikiwemo matumizi ya silaha kwenye maeneo ambayo hayakuhitajika.
Alisema ipo haja kwa Rais Magufuli kuwaeleza watanzania kuhusiana na baadhi ya maofisa wa ulinzi na usalama waliovamia kituo cha Luninga cha Clouds wakiwa na silaha na walio mtishia bastola Nape kama amewatuma na kama hakuwatuma pia aeleze hadi sasa ameelekeza wachukuliwe hatua gani, akiwa yeye ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.
Aidha alitumia nafasi hiyo kumpa pole kwa wanahabari na Nape kutokana na mambo mbalimbali yanayowakuta, na kuwataka Watanzania kutarajia kuwashwa moto katika Bunge la Bajeti linalotarajia kuanza hivi karibuni katika kujadili mambo mbalimbali yanayotokana na utendaji wa Serikali.
"Naamini safari hii hatutakuwa wabunge wa Chadema au wa vyama vya upinzani pekee bali naamini safari hii Bunge litakuwa kitu kimoja katika kuchukua hatua wakiwemo wabunge wa CCM," alisema.
Kuhusu wabunge walioteuliwa kushiriki katika uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, aliwataja walioteuliwa kutoka katika chama hicho kuwa ni Lawrence Macha na Ezekia Wenje.
Alibainisha kuwa wagombea hao walipatikana kutokana na vikao vya siku mbili vya Kamati Kuu ya Chadema vilivyo fanyika hivi Machi 22 na 23 mwaka huu.