Na Raymond Mushumbusi WHUSM
Serikali kupitia Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo imeanza rasmi kuandaa Sera ya Lugha ambayo itatoa muongozo kwa taifa kuhusu masuala yote ya maendeleo ya Lugha nchini ikiwemo Lugha ya Taifa ya Kiswahili.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia James Wambura wakati akifungua kongamano la Lugha ya Kiswahili liliofanyika katika Chuo cha KumbuKumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Anastazia Wambura amesisitiza kuwa kwa kipindi kirefu sana kumekuwa na uhitaji wa Sera ya Lugha ambayo itasaidia katika ukuaji na matumizi sahihi ya Lugha hasa Lugha ya Taifa ya Kiswahili.
“Kwa hivi sasa rasimu ya awali imeandaliwa na tunaendela kupokea maoni kutoka kwa wadau na kuyachambua” Alisistiza Mhe. Anastazia.
Ameeleza kuwa Sera ya Lugha itasaidia Lugha za Asilia, Lugha za alama , maandishi ya nukta nundu na Lugha za kigeni kuwekewa mkakati wa kuzishughulikia na kuzitumia kwa kukidhi mahitaji ya maendeleo endelevu ya Taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Lugha kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi Shani kitogo ameeleza kuwa mchakato wa kupokea maoni unaendelea na amewaomba wadau wa Lugha hasa Lugha yetu adhimu ya Kiswahili kuendelea kutoa maoni yao kwa ajili ya kupata Sera ya Lugha iliyo bora na itakayosaidia katika maendeleo na ukuaji wa Lugha nchini.
“Niwaombe wadau wa Lugha nchini waendelee kuleta maoni yao kwetu ili kuweze kufanikisha kupata Sera ya Lugha kwa Maendeleo ya Taifa Letu” Alisisitiza Bibi Shani.
Aidha Mwenyekiti wa Chama cha wanafunzi wa Kiswahili Vyuo vikuu Afrika Mashariki (CHAWAKAMA) Bw. Byatato Awadh ameishukuru Serikali ya waamu ya Tano kupitia Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kusikia kilio cha muda mrefu cha wadau wa Lugha kwa kuanza kuandaa Sera ya Lugha itakayoleta maendeleo katika ukuaji wa Lugha nchini.
“ Niishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa sikivu kwa wananchi na wadau wa maendeleo na tunaahidi kutoa ushirikiano katika uandaaji wa Sera hii ya Lugha”Alisisitiza Bw Byabato.
MWISHO.