Na Mwandishi Wetu
Serikali kupitia Wizara ya Ujezi Uchukuzi na Mawasilano imebariki uzinduzi wa televisheni mpya ya kidigitali kutoka kampuni ya Startimes Tanzania.
Akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof Makame Mbarawa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bibi. Maria Sasabo amesema Serikali imefarijika sana na ubunifu kutoka kwa kampuni ya StarTime Tanzania kwa kuanzisha televisheni ya kidigitali isiyotumia kinga’muzi kupata matangazo ya channeli mbalimbali.
“Hii ni fursa kwa watanzania kujipatia televesheni hizi ambazo ziko katika teknolojia ya hali juu sana ambazo zitasaidia Tanzania kuingia katika ulimwengu mpya wa mapinduzi ya sekta ya Habari na Mawasiliano” alisema Bibi. Maria.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa StarTimes Tanzania Bw. Leo Liao amesema kuwa StarTimes imelazimika kutoa televisheni hizo za kisasa ili kuendana na ukuaji wa teknolojia ambapo wateja wataweza vipindi vinavyoenda na wakati katika ubora wa hali ya juu.
“Tutahakikisha tunawapa wateja wetu vipindi vyenye ubora na muonekano mzuri ambao wataufurahia ulimwengu wa Digitali unaoendelea kubadilika kila kukicha duniani” alisistiza Bw. Liao.
Ameongeza kuwa televisheni hizo zimetengenezwa katika ubora unaotakiwa na ni rafiki kwa mazingira na zimezingatia matumizi madogo ya umeme na zinapatikana kwa bei nafuu ukilinganisha na televisheni kutoka makampuni mengine.
Televisheni hizo za kidigitali zinaonesha zaidi ya channeli 100 za kitaifa na kimataifa kuanzia habari, muziki, michezo, sinema, thamthilia,katuni, filamu na vipindi vya Dini.
MWISHO.
Mkurugenzi Mkuu wa StarTimes Tanzania Bw. Leo Liao(kushoto) akikabidhi zawadi ya moja ya televisheni za kidigitali yenye upana wa inchi 40 kwa mshindi wa televisheni hiyo Bw.John Paul wakati wa hafla ya uzinduzi wa televisheni hizo uliofanyika Novemba 16,2016 Jijini Dar es Salaam.