TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU ATINGA BANDARI YA TANGA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo jioni (Ijumaa, Februari 19, 2016) amekagua bandari ya Tanga na kumtaka Mkuu wa Bandari ya Tanga (Port Master), Bw. Henry Arika amletee maelezo juu ya ukiukwaji wa manunuzi ya tishari ifikapo kesho (Jumamosi) saa 6 mchana.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili Tanga leo mchana ili kushiriki mazishi ya baba mzazi wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu yaliyofanyika kwenye makaburi ya Mchukuuni, Tanga, aliamua kuzuru bandari hiyo kabla ya kuelekea uwanja wa ndege akiwa njia njiani kurejea Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo fupi, Waziri Mkuu alikataa kuingia ofisini (bandarini) na akataka apelekwe mahali tishari tatu za bandari hiyo zilipo. Katika maswali aliyoulizwa na Waziri Mkuu, Bw. Arika alikiri kuwa matishari hayo hayafanyi kazi kama inavyotakiwa kwa sababu yanasubiri kusukumwa na tugboat (meli ndogo).