Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Agenes Mtawa akimkabidhi vitanda Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Kibiti, Ayub Ngereza kutokana na hospitali ya halmashauri hiyo kuwa na upungufu wa vitanda vinavyotumiwa na kinamama wakati wa kujifungua. Mhandisi Ngereza amepokea msaada wa vitanda hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Kibiti.
NA JOHN STEPHEN, MNH
KATIKA kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji huduma ya afya ya uzazi kwa akina mama, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo Januari 27, 2017 imetoa msaada wa vitanda viwili vya kujifungulia kwa Hospitali ya Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.
Akikabidhi vitanda hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili , Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga, Agnes Mtawa, (pichani anayezungumza na waandishi), amesema lengo ni kuboresha huduma za afya na kumuwezesha mama kujifungua katika mazingira salama.
"Wenzetu wanahuitaji mkubwa wa vitanda vya kujifungulia hivyo tumeona tuwasaidie, natoa wito kwa Watanzania watambue kwamba hospitali hizi ni za kwetu na zinawahudumia Watanzania hivyo wale wenye nafasi ya kusaidia ni vema wakafanya hivyo ili kuendelea kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto" amesema Sister Mtawa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Huduma za Uuguzi na Ukunga tatizo la ukosefu wa vitanda husababisha Mkunga kupata shida wakati mama anapojifungua.
Naye Mhandisi Ujenzi wa Halmashauri ya Kibiti, Ayub Ngereza akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa wilaya ya Kibiti, ameushukuru uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa msaada huo kwani utasaidia kuboresha huduma za afya.
Hivi karibuni Hospitali ya Taifa Muhimbili ilikabidhi msaada wa vitanda vitano vya kujifungulia kwa Hospitali ya wilaya ya Mafya ambapo kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Abdalah Bhai walihitaji vitanda vitano ambao ulikidhi mahitaji.
Mhandisi Ngereza akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya kukabidhiwa vitanda hivyo na uongozi wa hospitali hiyo.
Baadhi ya wafanyakazi wa Halmashauri hiyo wakipakia vitanda hivyo kwenye gari leo