NA LILIAN LUNDO - MAELEZO
CHAMA cha Kutetea Abiria Tanzania (CHAKUA) kimeiomba Serikali kuongeza nguvu na kuhakikisha matumizi ya tiketi za elekroniki katika sekta ya usafirishaji nchini yanakuwa ya lazima.
Hayo yamesemwa na Afisa Msimamizi wa Chama hicho ambaye anasimamia Mkoa wa Dar es Salaam Mark Serra, alipokuwa akisoma taarifa ya chama hicho kwa waandishi wa habari leo, Jijini Dar es Salaam.
“Chakua imekuwa ikifuatilia kwa karibu mfumo huu na kubaini una manufaa makubwa sana kwa abiria ambapo watatozwa nauli halali iliyoidhinishwa na Sumatra ambazo ndizo bei elekezi kwa mujibu wa sheria,” alifafanua Serra.
Aliendele kusema kuwa kwa kutumia tiketi za Kielekroniki itawalazimu wamiliki wa vyombo vya usafiri kutokupandisha nauli katika kipindi cha mvua au jua kali, kipindi cha wanafunzi wapotoka vyuoni au mashuleni pamoja na kipindi cha sikukuu au mwanzoni mwa mwaka, ambapo mabasi mengi huita vipindi hivyo ni vya kuvuna abiria.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama hicho Hassan Mchanjama amesema kuwa mfumo huo utamnufaisha abiria na kuokoa muda wa kwenda kwenye vituo vya mabasi kwa ajili ya kukata tiketi badala yake mfumo huu utamuwezesha abiria kukata tiketi akiwa nyumbani, ofisini au sehemu yoyote aliyopo kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Aliongeza kuwa mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu za abiria pindi inapotokea ajali kujua abiria wangapi wamepoteza maisha, waliopata ulemavu pamoja na waliopoteza mali zao, ambapo kwa mfumo unaotumika sasa hivi ni vigumu kupata takwimu na taarifa sahihi za abiria.
Hivyo basi kupitia mfumo huo wa kielekroniki CHAKUA itakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kutekeleza jukumu lake la kumtetea abiria pindi anapopata tatizo kwa kuwa itakuwa na taarifa sahihi za abiria.