Maofisa wa taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika (WAF) Anna Salado na Alicia (kushoto) wakipata maelezo ya fugaji nyuki katika msitu wa hifadhi wa Pugu.
WANAWAKE wanaofuga nyuki wataokoa hekta 7,270 za misitu ya hifadhi ya Pugu na Kazimzumbwi, imefahamika.
Misitu hiyo, ambayo ni miongoni mwa Misitu ya Hifadhi 486 iliyopo nchini, imekuwa hatarini kutoweka kutokana na shughuli za kijamii hususan uvamizi wa mipaka na ukataji wa miti kwa ajili ya uchomaji mkaa ambao kwa muda mrefu umekuwa ukifanywa na wananchi mbalimbali.
Meneja wa Misitu hiyo kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Mathew Mwanuo, anasema kwamba, misitu hiyo iliyopo katika wilaya za Ilala mkoani Dar es Salaam na Kisarawe mkoani Pwani, imekuwa hatarini kutoweka licha ya jitihada za serikali za kukabiliana na wavamizi hao.
“Lakini sasa miradi hii ya ufugaji nyuki inayowahusisha wanawake wa Pugu na Kisarawe itakuwa mkombozi kwa sababu wananchi wenyewe wanahusishwa moja kwa moja na suala la ulinzi,” anasema Mwanuo wakati akiwaelekeza wageni kutoka taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika (WAF) kutoka nchini Hispania waliotembelea miradi hiyo hivi karibuni.
Mwanuo anasema kwamba, ndani ya misitu hiyo ya hifadhi kuna jumla ya vikundi vinne vya akinamama vinavyojihusisha na ufugaji wa nyuki wa kisasa, ambapo viwili vinafadhiliwa na mradi wa Green Voices Tanzania na viwili vinafadhiliwa na TFS.
Anna Salado akiwa msituni kuangalia ufugaji wa nyuki kwenye hifadhi ya Pugu.“Kazi ni kubwa katika kuilinda misitu hii, tunao askari wetu wanaozunguka humu, lakini hawatoshi kuweza kuzunguka maeneo yote na ndiyo maana huko nyuma watu walikuwa wakivamia kukata miti na kuchoma mkaa.
“Zamani ulikuwa ukipita pembeni unaona misitu inapendeza, lakini ukiingia ndani kulikuwa na watu wanachoma mkaa huku mambo mengine yakiendelea kama uuzwaji wa vinywaji na kadhalika… yaani hali ilikuwa mbaya sana,” anasema.
Mshiriki kiongozi wa miradi hiyo ya ufugaji wa nyuki chini ya Green Voices, Monica Kagya, anasema kwamba, anaishukuru taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika (WAF) kwa kumwezesha yeye na wenzake 14 kupata mafunzo nchini Hispania mapema mwaka huu ili kuwapa uwezo wanawake kushiriki shughuli za utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mshiriki kiongozi wa mradi wa ufugaji nyuki Pugu na Kazimzumbwi, Monica Kagya, akitoa maelezo kwa wageni (hawapo pichani).“Nilichagua mradi huu wa ufugaji wa nyuki kwa sababu naamini misitu hii ya Pugu na Kazimzumbwi inaweza kuokolewa kutoka katika hatari ya kutoweka, lakini ndiyo mapafu halisi ya Dar es Salaam kwa kuwa inasaidia kutoa hewa ya oksijeni kwenye jiji hilo ambalo idadi ya watu inaongezeka kila siku pamoja na shughuli za uchumi, vikiwemo viwanda,” anasema Kagya.
Bi. Kagya, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa TFS, anasema kwamba, ili kutunza mazingira ni muhimu kuwashirikisha wanawake ambao ndio wahanga wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi kutokana na kushughulikia majukumu yote ya nyumbani ikiwemo utafutaji wa nishati za kupikia, hususan kuni na mkaa.
Anasema kwamba, vikundi vyote viwili vinavyotekeleza mradi wa Green Voices vipo katika msitu wa hifadhi wa Pugu ambapo kimoja kina mizinga 12 na kingine kina mizinga 52.
“Vikundi vingine viwili vinavyofadhiliwa na TFS vipo katika msitu wa hifadhi wa Kazimzumbwi,” anasema.
Mkurugenzi wa Mfuko wa Wanawake Afrika, Anna Salado, ambaye aliwaongoza wenzake kukagua mizinga pamoja na kushuhudia zoezi la urinaji wa asali katika msitu wa Kazimzumbwi, alieleza kufurahishwa kwake na jitihada za kutunza mazingira pamoja na mafanikio ya mradi huo.
“Hakika jitihada hizi ni kubwa, tumefurahi sana kuona akinamama wanakuwa mstari wa mbele kupambana na uharibifu wa mazingira lakini wakati huo huo wanafanya miradi inayoweza kuwakwamua kiuchumi,” alisema Bi. Salado.
Meneja wa Misitu ya Hifadhi ya Pugu na Kazimzumbwi, Mathew Mwanuo, akitoa maelezo na changamoto zinazowakabili.Maofisa wa Mfuko wa Wanawake Afrika unaofadhili mradi wa Green Voices nchini Tanzania wakiwa wanakaribishwa na wanawake wafuga nyuki katika misitu ya Pugu na Kazimzumbwi kabla ya kuingia msituni kuangalia shughuli za ufugaji huo wa nyuki.
Alicia (wa pili kulia), mratibu wa mradi wa Green Voices kutoka Hispania, akiangalia sega la nyuki katika msitu wa Kazimzumbwi.
Alphonce Matata akiwasha moto kabla ya kuanza shughuli ya urinaji asali.
Bi. Salado ameahidi kwamba, katika awamu ya pili ya mradi wa Green Voices, watajitahidi kuwawezesha washiriki katika suala zima la kuongeza uelewa wa madhara ya uharibifu wa mazingira pamoja na kuangalia uwezekano wa kutatua changamoto zinazowakabili, zikiwemo za vitendea kazi kama mavazi pamoja na mizinga ya kutosha.
Mradi wa Green Voices unatekelezwa nchini Tanzania pekee chini ya ufadhili wa WAF na ulizinduliwa jijini Dar es Salaam Julai 11, 2016 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa sambamba na rais wa taasisi ya WAF ambaye pia ni makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Maria Teresa Fernandez e la Vega, ambaye tayari amekwisharejea jijini Madrid.
Mratibu wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, amepongeza jitihada za akinamama hao na kuwataka wawe walimu wa jamii nzima ili kuokoa misitu hiyo.
Bi. Secelela, ambaye ni mwanahabari kitaaluma, amesema kwamba, walau hali sasa inaonyesha kubadilika kuliko ilivyokuwa siku za nyuma ambapo misitu hiyo ilikuwa inakaribia kutoweka.
“Nilikuja huku miaka mitano iliyopita wakati nikiandika habari za mazingira, hali ilikuwa mbaya sana, maana katikati yam situ nasikia kuna watu waliweka mpaka baa, lakini sasa kwa kuanzisha miradi hii ambayo inawataka wanamradi kuzungukia kila wakati kwenye mizinga yao kutawakimbiza wavamizi wote,” alisema.
Ameongeza kwamba, uwepo wa misitu hiyo ni muhimu kwa sababu ndiyo ‘mapafu ya Dar es Salaam’ katika kukabiliana na hewa chafu inayozalishwa jijini humo.
-- Brother Danny Blog (Kisima cha Hekima na Busara)