Silaha mbalimbali zilizo kamatwa katika tukio la kuuwawa kwa majambazi wilayani Chunya mkoani Mbeya Aprili 27 mwaka huu. JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kuwaua watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi katika majibizano ya kurushiana risasi wakiwa katika majaribio ya kufanya uhalifu kwenye duka la Bia la Jumla. Akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Butusyo Mwambelo, alisema tukio hilo lillitokea juzi majira ya saa mbili usiku katika kijiji cha Matundasi Wilaya ya Chunya Mkoani hapa. Mwambelo alisema siku ya tukio majambazi hao walikuwa watano na walibebana kwenye pikipiki mbili ambapo majambazi watatu walipanda pikipiki moja huku wengine wawili wakiwa wamepanda nyingine. Alisema Jeshi la Polisi lilipata taarifa ya kiinterensia na kufanikiwa kujipanga ili kukabiliana na majambazi hao ambapo katika majibizano ya risasi jambazi mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Baraka anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 35 – 38 mkazi wa Makongolosi na fundi ujenzi aliuawa kwa kupigwa risasi tumboni na mgiuuni. Alisema marehemu baada ya kukaguliwa alikutwa na silaha aina ya SMG yenye namba 1996 AFU 1120 ikiwa na risasi 26 kwenye magazine,na kwamba majambazi wengine wanne walifanikiwa kukimbia kuelekea Kijiji cha Matondo na ndipo askari waliendesha msako kuwatafuta. Alisema baada ya majambazi kuwaona askari waliwasha pikipiki zao kwa nia ya kukimbia huku wakirusha risasi ovyo ndipo Polisi walijibu mapigo na kufanikiwa kuwaua majambazi wawili na kukamata pikipiki moja yenye namba za usajili MC 761 AFS aina ya Sanlg iliyokuwa ikitumiwa na majambazi hao pamoja na Begi moja lenye tochi na Panga.. Alisema majambazi wengine wawili walifanikiwa kukimbilia kusiko julikana ambapo Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali likishirikiana na wananchi ili kuwakamata waliotoroka na kwamba miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya. Aliongeza kuwa majina ya miili ya majambazi wawili hayajafahamika ambapo alitoa wito kwa wananchi kufika katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya kuwatambua ikiwa ni pamoja na kuchukua miili yao baada ya kufuata utaratibu baada ya kuwatambua kwa ajili ya kuwazika kutokana na Hospitali hiyo kukabiliana na changamoto ya Chumba cha kuhifadhia maiti. Aidha Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Butusyo Mwambelo anatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za siri ili kuzuia vitendo vya kihalifu mapema kabla ya kutokea. |